Waziri wa Nishati na Madini. George Simbachawene, akisisitiza jambo kwa wanafunzi kabla ya kuwakabidhi Nyaraka za Ufadhili kwa ajili ya masomo yao nchini China.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, (Kulia) akizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya Watumishi wa Wizara na wanafunzi waliopata ufadhili wa masomo katika ngazi za Shahada za Uzamivu (Phd) na Uzamili (Masters), katika masuala ya mafuta na gesi nchini China.
Baadhi ya wanafunzi 22 waliopata nafasi za masomo ya shahada za Uzamili na Shahada ya Uzamivu wakimsikiliza kwa kwa makini Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene.
Waziri akiwakabidhi nyaraka za kusafiria na zenye maelezo baadhi ya wanafunzi waliopata ufadhili wa masoma katika masuala ya mafuta na gesi nchini China.Katikakati ni Kaimu Kamishna wa Nishati na Maendeleo ya Petroli, James Andilile.
Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene akiwakabidhi wanafunzi 22 wa Kitanzania Nyaraka za Ufadhili wa kusoma masuala ya mafuta na gesi nchini China.
Na Clinton Ndyetabula.
Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene, amewakabidhi Nyaraka za Ufadhili na kuwaaga wanafunzi 22 wa Kitanzania wanaokwenda masomoni nchini China, kusoma masuala ya mafuta na gesi katika ngazi za Shahada za Uzamivu (Phd) na Uzamili (Masters).
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi Nyaraka hizo, Makao Makuu ya Wizara, Jijini Dar es Salaam, leo, Simbachawene amewataka wanafunzi hao kutumia fursa hiyo kusoma kwa bidii ili hatimaye waweze kusaidia Taifa katika kuendeleza sekta ndogo ya gesi ikiwemo kuanzisha vyanzo mbadala vya nishati ya umeme , kuongeza usimamizi ili kuendana na kasi ya ukuaji wa sekta hiyo, na kusaidia katika kuondoa changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
“Kama mnavyoelewa Wizara yetu ni miongoni mwa Wizara zilizo katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) katika sekta ya Nishati. Mpango huu unategemea kutoa matokeo makubwa ya haraka, na hili kutekeleza ipasavyo tunahitaji wataalamu wazalendo waliobobea katika fani za ,mafuta na gesi asilia” alisema Simbachawene.
“Ni matumaini yangu kuwa mtatumia vizuri fursa mliyopata, mtajifunza kwa bidii na kuiwakilisha nchi yetu vizuri na kuleta teknolojia zitakazosaidia kupata ufumbuzi au mapendekezo ya namna ya kutatua changamoto zilizopo katika sekta hii”alieleza Simbachawene.
Aidha, Waziri alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa kuwawezesha Watanzania kusoma masuala ya mafuta na gesi tangu mwaka 2013 na kuongeza kuwa , serikali hiyo imeahidi kuendelea kutoa ufadhili kwa watanzania katika ngazi za Shahada ya Uzamivu na Uzamili hadi ifikapo mwaka 2019.
Aidha, Simbachawene ameeleza kuwa, Wizara ilipokea jumla ya maombi 187 na kati yao, waombaji 33 waliokidhi vigezo walichunjwa na Serikali ya Watu wa China na kupatikana washindi 22.
Clinton Ndyetabula ni Mwanafunzi ambaye yuko katika Mafunzo ya Vitendo, Wizara ya Nishati na Madini.
0 comments:
Post a Comment