Rais Jakaya Kikwete.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam.
RAIS Jakaya Kikwete amesema madai kuwa elimu
inayotolewa Tanzania ni duni ni potofu kwani wahitimu wake wanakubalika duniani.
Akihutubia Mkutano Mkuu wa Nane wa Baraza la Taifa la
Biashara (TNBC) uliofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam, Rais Kikwete alisema
badala yake, tatizo liko kwenye kuwaandaa wahitimu kukidhi matakwa ya soko la
ajira la ndani na la kimataifa.
“Elimu yetu ni bora na inakubalika popote duniani...wahitimu
wanaweza kufanya kazi katika nchi yoyote, kinachotakiwa ni kuwapatia ujuzi wa
kutosha kukidhi matakwa ya soko la ajira,” Rais Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Baraza hilo aliwaambia wadau wa mkutano huo toka sekta ya umma na
binafasi ambao hutoa ajira kwa wahitimu wa vyuo.
Takwimu zinaonyesha kwamba vijana wanaoingia kwenye
soko la ajira kila mwaka nchini ni kati ya 800,000 hadi 1,000,000 na
wanapigania nafasi za ajira zisizozidi 60,000 katika sekta ya umma na nafasi
takribani 300,000 katika sekta binafsi.
Dkt. Kikwete alisema serikali inajitahidi kuboresha mazingira
ya kufanya biashara na kuvutia wawekezaji na kuomba mchango wa kila mdau
kutumia fursa na raslimali zilizopo nchini kuzalisha mali na kuongeza ajira
katika sekta ya umma na sekta binafsi.
Rais aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa kila
anayestahili kulipa kodi afanye hivyo na kusisitiza kuwa “serikali haiko tayari
kuona watu wanakwepa kulipa kodi.”
Akitoa mfano alisema kama wadau wa sekta ya usafiri wa
ndege wanaona kodi wanazotozwa ni kubwa ni vyema wakakaa na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) wakubaliane lakini siyo kuchukua uamuzi wa kutolipa kodi.
Kuhusiana na mapambano ya rushwa alisema Tume ya
Kupambana na Kuzuia Rushwa (PCCB) ijidhatiti vya kutosha kwa weledi na kwa
mujibu wa sheria ili uwepo ushahidi wa kuiridhisha mahakama kumtia hatiani
mshitakiwa.
“Mnapokwenda mahakamani mkashidwa mara kwa mara, zoezi
hili la kupambana na kuzuia rushwa halitofanikiwa,” alieleza.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara
ya Mali Asili na Utalii, Dkt. Adelhelm Meru alisema ingawa utalii unazidi
kuimarika na kuchangia pato la taifa,
unakumbwa na tatizo la ujangili unaoangamiza tembo na faru.
Katika kukabiliana na tatizo hilo, alisema vifaa na
askari vitaongezwa na kuwa patajengwa minara ya kuimarisha ulinzi katika mbuga
za Serengeti na Ruaha.
Aliwataka wananchi kutochunga mifugo katika mbuga hizo
kwani serikali haitoruhusu vurugu na uharibifu unaofanywa katika mbuga za
wanyama uendelee.
0 comments:
Post a Comment